Luke 2

Kuzaliwa Kwa Yesu

(Mathayo 1:18-25)

1 aSiku zile Kaisari Augusto alitoa amri kwamba watu wote waandikishwe katika ulimwengu wa Kirumi. 2 b(Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyofanyika wakati Krenio alikuwa mtawala wa Shamu
Shamu inamaanisha Syria.
).
3Kila mtu alikwenda kuandikishwa katika mji wake alikozaliwa.

4 dHivyo Yosefu akapanda kutoka mji wa Nazareti ulioko Galilaya kwenda Uyahudi, mpaka Bethlehemu, mji wa Daudi, kwa sababu yeye alikuwa wa ukoo na wa nyumba ya Daudi. 5 eAlikwenda huko kujiandikisha pamoja na Maria, ambaye alikuwa amemposa naye alikuwa mjamzito. 6Wakiwa Bethlehemu, wakati wa Maria wa kujifungua ukawa umetimia, 7 fnaye akamzaa mwanawe, kifungua mimba. Akamfunika nguo za kitoto na kumlaza katika hori ya kulia ngʼombe, kwa sababu hapakuwa na nafasi katika nyumba ya wageni.

Wachungaji Na Malaika

8Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku. 9 gGhafula tazama, malaika wa Bwana akawatokea, nao utukufu wa Bwana ukawangʼaria kotekote, wakaingiwa na hofu. 10 hLakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama nawaletea habari njema za furaha itakayokuwa kwa watu wote. 11 iLeo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo
Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.
Bwana.
12 kHii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori ya kulia ngʼombe.”

13 lGhafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema,

14 m“Atukuzwe Mungu juu mbinguni,
na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”
15Hao malaika walipokwisha kuondoka na kwenda zao mbinguni, wale wachungaji wakasemezana wao kwa wao, “Twendeni Bethlehemu tukaone mambo haya ya ajabu yaliyotukia, ambayo Bwana ametuambia habari zake.”

16 nHivyo wakaenda haraka Bethlehemu, wakawakuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori la kulia ngʼombe. 17 oWalipomwona yule mtoto, wakawaeleza yale waliyokuwa wameambiwa kuhusu huyo mtoto. 18Nao wote waliosikia habari hizi wakastaajabia yale waliyoambiwa na wale wachungaji wa kondoo. 19 pLakini Maria akayaweka mambo haya yote moyoni mwake na kuyatafakari. 20 qWale wachungaji wakarudi, huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa ajili ya mambo yote waliyokuwa wameambiwa na kuyaona.

21 rHata zilipotimia siku nane, ulikuwa ndio wakati wa kumtahiri mtoto, akaitwa Yesu, jina alilokuwa amepewa na malaika kabla hajatungwa mimba.

Yesu Apelekwa Hekaluni

22 sUlipotimia wakati wa utakaso wake Maria kwa mujibu wa Sheria ya Mose, basi Yosefu na Maria walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Bwana 23 t(kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana, kwamba, “Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Bwana”), 24 una pia kutoa dhabihu kulingana na yale yaliyonenwa katika Sheria ya Bwana: “Hua wawili au makinda mawili ya njiwa.”

25 vBasi alikuwako huko Yerusalemu mtu mmoja jina lake Simeoni, ambaye alikuwa mwenye haki na mcha Mungu, akitarajia faraja ya Israeli, na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. 26 wRoho Mtakatifu alikuwa amemfunulia kuwa hatakufa kabla hajamwona Kristo wa Bwana. 27 xSimeoni, akiwa ameongozwa na Roho Mtakatifu, alikwenda Hekaluni. Wazazi walipomleta mtoto Yesu ili kumfanyia kama ilivyokuwa desturi ya Sheria, 28ndipo Simeoni akampokea mtoto mikononi mwake na kumsifu Mungu, akisema:

29 y“Bwana Mwenyezi, kama ulivyoahidi,
sasa wamruhusu mtumishi wako
aende zake kwa amani.
30 zKwa maana macho yangu yameuona wokovu wako,
31ulioweka tayari machoni pa watu wote,
32 aanuru kwa ajili ya ufunuo kwa watu wa Mataifa
na kwa ajili ya utukufu kwa watu wako Israeli.”
33Naye Yosefu na mama yake mtoto wakastaajabu kwa yale yaliyokuwa yamesemwa kumhusu huyo mtoto. 34 abKisha Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, “Mtoto huyu amewekwa kwa makusudi ya kuanguka na kuinuka kwa wengi katika Israeli. Atakuwa ishara ambayo watu watanena dhidi yake, 35 acili mawazo ya mioyo mingi yadhihirike. Nao upanga utauchoma moyo wako.”

36 adTena alikuwako Hekaluni nabii mmoja mwanamke, jina lake Ana binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa mzee sana; naye alikuwa ameolewa na kuishi na mume kwa miaka saba tu, kisha mumewe akafa. 37 aeHivyo alikuwa mjane na umri wake ulikuwa miaka themanini na minne. Yeye hakuondoka humo Hekaluni usiku wala mchana, bali alikuwa akimwabudu Mungu, akifunga na kuomba. 38 afWakati huo huo, Ana alikuja akaanza kusifu, akimshukuru Mungu na kusema habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wakitarajia ukombozi wa Yerusalemu.

39 agYosefu na Maria walipokuwa wamekamilisha mambo yote yaliyotakiwa na Sheria ya Bwana, walirudi mjini kwao Nazareti huko Galilaya. 40 ahNaye yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu, akiwa amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.

Kijana Yesu Hekaluni

41 aiKila mwaka Yosefu na Maria mama yake Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka. 42Yesu alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, walipanda kwenda kwenye Sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. 43 ajBaada ya Sikukuu kumalizika, wakati Yosefu na Maria mama yake walipokuwa wakirudi nyumbani, Yesu alibaki Yerusalemu lakini hawakutambua. 44Wao wakidhani kuwa yuko miongoni mwa wasafiri, walienda mwendo wa kutwa nzima. Ndipo wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa zao na marafiki. 45Walipomkosa walirudi Yerusalemu ili kumtafuta. 46Baada ya siku tatu wakamkuta ndani ya Hekalu, akiwa ameketi katikati ya walimu wa sheria, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47 akWote waliomsikia walistaajabishwa na uwezo wake mkubwa wa kuelewa, na majibu aliyoyatoa. 48 alYosefu na Maria mama yake walipomwona walishangaa. Mama yake akamuuliza, “Mwanangu, mbona umetufanyia hivi? Tazama, mimi na baba yako tumekuwa tukikutafuta kwa wasiwasi mkubwa kila mahali.”

49 amYesu akawaambia, “Kwa nini kunitafuta? Hamkujua kwamba imenipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?”

50 anLakini wao hawakuelewa maana ya lile alilowaambia.

51 aoNdipo akashuka pamoja nao hadi Nazareti, naye alikuwa mtiifu kwao. Lakini mama yake akayaweka moyoni mwake mambo haya yote. 52 apNaye Yesu akakua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.

Copyright information for SwhNEN